Wednesday, October 14, 2015

MAFUTA NA GESI TISHIO KWA SEKTA NYINGINE


Na Sylvia Mwehozi
Shughuli za uchimbaji wa mafuta na  gesi ni moja ya sekta ambazo  zinakua kwa kasi katika nchi kadhaa barani  Afrika ambazo zimegundua uwepo wa nishati hiyo. Ghana ni mojawapo ya nchi ambayo imeanza shughuli za uzalishaji miaka mitano iliyopita.  Mkoa wa Magharibi ambao upo kilometa 182 kutoka mji mkuu wa Accra ndiko shughuli za uchimbaji zinafanyika.
Hivi karibuni nilitembelea wilaya ya Sekondi-Takoradi iliyoko mkoani humo na kufika katika eneo ambalo Gesi inazalishwa, ambapo kwa mujibu wa wakazi wa mji huu ,  kumekuwa na mabadiliko ya shughuli za kiuchumi, mwingiliano mkubwa wa watu wa kutoka sehemu tofauti na kuibuka kwa fursa mbalimbali.
Suala la Idadi ya watu wanaokimbilia katika  mkoa wa  Magharibi nchini Ghana kutokana na kuwepo kwa shughuli za uchimbaji wa gesi na mafuta, imezidi kuongezeka na kuleta wasiwasi kwa wenyeji lakini pia ikihatarisha kudidimia kwa sekta nyingine za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2010 , mkoa huo ulikuwa na wakazi laki mbili lakini hivi sasa idadi hiyo imezidi kuongezeka na kufikia wakazi laki tano. Idadi hiyo inatajwa kuongezeka kwa sababu ya kuanza kwa shughuli za uchimbaji wa gesi , ambazo zimeibua fursa nyingine, kama ongezeko la ajira , na shughuli nyingine za kiuchumi.
Katika mazungumzo na ujumbe wa waandishi wa habari , Naibu waziri wa mkoa huo Paul Evans Aidoo anasema kuwa wasiwasi umekuwa mkubwa kwa sababu mkoa huo wa Magharibi ndo kitovu cha uchumi wa nchi kwa hivi sasa. ‘Kutokana na ugunduzi wa gesi na mafuta, watu wengi kutoka kaskazini mwa mkoa huu wanashuka chini, eneo la pwani, kwa kufanya hivyo tunahofia kuwa sekta nyingine kama kilimo zitakufa’ alimalizia naibu waziri Aidoo ambaye pia anakaimu umeya wa mkoa huo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, tayari kumeanzishwa mpango mkakati ambao utawasaidia wananchi kuelewa umuhimu wa kushiriki katika uzalishaji wa sekta nyingine badala ya kukimbilia mkoa huo kwa sababu ya mafuta.
Naibu Waziri  wa mkoa wa Magharibi nchini Ghana , Amos Anyimadu akizungumza na baadhi ya wandishi wa habari walipomtembelea ofisini kwake.
Kauli yake inaungwa mkono na Amos Anyimadu, mwanazuoni na mtaalamu wa masuala ya siasa , Kwanza anadiriki kusema kuwa wananchi walikuwa na matarajio makubwa baada ya ugunduzi wa gesi na mafuta, hata hivyo matarajio hayo yanapingana na uhalisia uliopo na hii inachangiwa na sababu kubwa ya kuiona sekta hiyo ya gesi kama mkombozi pekee wa uchumi. ‘’Vyombo vya habari vinapaswa kufanya kazi yake ipasavyo, kama nilivyowaambia mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009 wakati nilisikia kwenye radio moja kuwa Takoradi sasa ni mji wa mafuta, na kulikuwa na mabango kadhaa, yanayosema karibu! Karibu! mji wa mafuta Takoradi lakini nyie wenyewe mmetembea mmejionea hali ilivyo ’’ alisema Dr. Anyimadu.
Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, wananchi wanapaswa kuelimishwa kuwa sekta ya mafuta na gesi pekee haviwezi kuwa chanzo cha mapato na kuacha shughuli nyingine za kiuchumi.
Mtambo wa uzalishaji gesi wa Atuabo ulioko mkoa wa magharibi nchini Ghana
Moja ya mikakati ambayo imeanzishwa na serikali ya mkoa huo ni uanzishwaji wa taasisi ya Western Region coast foundation ambaye inalenga kuwa jukwaa la wadau wote wa mafuta, na gesi pamoja na wananchi kujadili mahitaji , fursa , changamoto na kuwezesha upatikanaji wa majibu juu ya mahitaji hayo.
Tangu kuanzishwa kwake majadiliano katika jumla ya jamii 177 yamefanyika na masuala 620 yakiibuliwa katika Nyanja za uchumi, afya, maji, elimu, miundombinu, mazingira na utawala bora.  Wananchi wa eneo hilo wanasema kuwa fursa zipo, hata hivyo wazawa wenyewe hawajawa tayari kuzitumia na matokeo yake wanaishia kulalamika kuwa wageni wanazichukua. Sylvia Ousu ni mwanamke mfanyabiashara katika eneo la market circle, anasema mwanzoni walikuwa na mategemeo makubwa waliposikia gesi, lakini sasa ni tofauti, biashara haiendi kwasababu watu wanalalamika hawana hela.
Hata hivyo anasema watu wanapaswa kuchangamkia fursa, ‘’ingawa fedha hakuna , lakini kama sisi wanawake tunapaswa kufanya kazi , kama hapa sokoni wanawake wengi wanafanya biashara , ni vizuri kuliko kutofanya kazi kabisa’’.
Mkoa wa magharibi sasa umekuwa lulu miongoni mwa maeneo ya uwekezaji nchini Ghana, gharama za maisha nazo zimezidi kupanda , kwa mfano chupa moja ya maji ya kunywa unaweza kuipata kwa cede 4 hadi 5 ambayo ni sawa na dola 1.4 moja ya marekani tofauti na hali ilivyo mji mkuu wa ACCRA ambako chupa ya maji unainunua kwa cede 1 hadi 2 sawa na dola 0.57 ya Marekani.
Tanzania ikiwa imeanza shughuli za uchimbaji inapaswa kujifunza kuwa wananchi wanahitaji elimu ya kutosha ya kuzingatia mchango wa sekta nyingine za kiuchumi badala ya kukimbilia mjini Mtwara pekee wakiwa na matarajio ya kupata ajira, na fursa nyinginezo na hivyo kuhatarisha uchumi kwa kuwa sekta nyingine zitakuwa hazizalishi


No comments:

Post a Comment