Tuesday, October 13, 2015

Uchimbaji wa madini wahatarisha zao la cocoa Ghana


Rehema Matowo, Mwananchi
Ghana. Zao la Cocoa ambalo linalimwa kwa wingi nchini Ghana lipo hatarini kutoweka  kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uchimbaji wa madini juu ya ardhi.
Kutokana na hali hiyo serikali ya Ghana na nchi nyingie za Afrika zimeshauriwa kujikita zaidi katika uchimbaji wa madini chini ya ardhi ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
Hayo  yamesemwa  na katibu mkuu wa Asasi isiyo ya kiserikali inayosimamia shughuli za wachimbaji wadogo wadogo wa madini katika eneo la Prectea Dominic Nyame wakati akizungumza na jopo la waandishi wa habari kutoka nchi za Tanzania,Uganda na Ghana waliotembelea eneo hilo kuona shughuli zinazofanywa na wachimbaji wadogowadogo .
Nyame alisema kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini juu ya ardhi unaoendelea katika eneo hilo umesababisha  viumbe hai  kutoweka ,vyanzo vya maji kama mito  na mabwawa kuwa na kemikali za sumu  pamoja na shughuli za kilimo kushindwa kuendelea.
“eneo hili lilikua na vyanzo 90 vya maji safi na salama lakini kutokana na uchimbaji wa madini juu ya ardhi umesababsha  vyanzo kukauka na kubaki kimoja huku vingine, maji  yake hayafai kwa matumizi kutokana na kemikali”alisema  Nyame.
Akizungumza na waandishi wa habari chief watatu kutoka Prestea Nana kwaw Nsowah  alisema  uchimbaji wa madini juu ya ardhi kwa kutumia kemikali  umesababisha maji kuwa na sumu  na kutofaa kwa matumizi ya  binadamu na viumbe hai.
Chief alisema licha ya eneo hilo kuchimbwa madini kwa miaka mingi wananchi walikua hawanufaiki nayo na kwamba tayari serikali ya Ghana imesikia kilio cha wananchi na kuingia makubaliano kati yake na mwekezaji ili wananchi waweze kunufaika na madini yanayopatikana katika maeneo yao.
Alisema kwa mwaka 2013/14 kampuni ya madini ya  Gold Star imetoa kiasi cha dola 30,000 kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo fedha ambazo zimetumika kujenga hospitali na kuwaondolea wananchi adha .
Aidha  alisema uchimbaji wa madini chini ya ardhi ukipewa kipaumbele  utapunguza uharibufu wa mazingira kwa zaidi ya asilimia themanini
Alisema ni wakati  wa nchi za Afrika kuachana na uchimbaji wa juu ya ardhi na badala yake wanapaswa kujikita katika uchimbaji wa chini ya ardhi ili kuzuia uharibifu mkubwa wa mazingira ambao madhara yake  ni makubwa.
Mmoja wa wakufunzi  kutoka nchini Tanzania  Deodatus  Mfugale  kutoka  chama cha waandishi wa habarai za mazingira  (JET), alisema  kampuni ,serikali za nchi husika zinapaswa kuhakikisha makampuni ya uchimbaji wa madini yanazingatia  taratibu za kimataifa za utunzaji wa mazingira.

Alisema serikali kupitia taasisi za kusimamia mazingira kwa nchi husika zinapaswa  kupitia upya sera zao pamoja na kufanya tathmini ya athari za mazingira kwa jamii.
Aidha  alizikosoa  serikali ambazo nchi zao zimebarikiwa  kuwa  na rasirimali nyingi  lakini zimeshindwa kuwa na mipango imara ya kuhifadhi mazingira kabla na baada ya shughuli za uchimbaji .

Mfugale  alisema  serikali hizo zinatakiwa kuweka sera mahususi zitakazo bana makampuni ya madini kabla ya kutoa leseni ya uchimbaji ili kulinda mazingira pamoja na madhara yoyote yanayoweza kusababishwa na shughuli za uchimbaji.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment