Monday, October 12, 2015

WANA MTWARA JIFUNZENI KUTOKA MJI WA TAKORADI

Leah Mushi

Wananchi wa mkoa wa MTWARA wameshauriwa kutumia fursa zilizopo kutokana na rasilimali ya gesi iliyopo mkoani kwao ili kujiletea maendeleo badala ya kutegemea kuletewa maendeleo na serikali peke yake.

Hayo yamesemwa na Dokta AMOS ANYIMADU ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya siasa pamoja na masuala ya mafuta na gesi barani Afrika.

Dokta ANYIMADU amesema wananchi wa MTWARA wanatakiwa kujifunza yaliyotokea katika mji ya TAKORADI ulioko Mkoa wa MAGHARIBI mwa GHANA ambao ulianza uchimbaji wa mafuta mwaka 2010 lakini matarajio ya wananchi ya kukuwa kwa mji huo hayajafikiwa na badala yake wananchi wamekuwa wakilalamikia hali ngumu ya maisha.

“Gesi peke yake haiwezi kubadilisha maisha ya watu, zipo fursa nyingi katika mikoa yenye mafuta na gesi ambazo ni pamoja na kuanzisha kwa mashamba yatakayo zalisha chakula kitakacho uzwa kwenye makampuni ya kigeni , kuanzishwa kwa maduka ya kufua nguo, kutoa huduma mbalimbali zikiwemo Bar na Hoteli”.

Pia amekumbusha kuwa wananchi wanatakiwa kuhakikisha huduma hizo watakazo toa zinakidhi viwango vya kimataifa na kwa wingi unaotakiwa ili makampuni hayo ya kigeni yaweze kutumia bidhaa hizo.

EVA AKOTO ni mmoja wa wafanyabiashara wa bidhaa za kuogea katika soko la Mzunguko lililoko mjini TAKORADI  amesema baada kugundulika na serikali kuamua kuchimba mafuta walikuwa wanatarajia maisha yatakuwa rahisi na huduma zote zitapatikana kwa urahisi kitu ambacho hakijatokea kwani kwa sasa maisha ya TAKORADI ni ya hali ya juu kuliko mji wowote nchini GHANA.

“Mfano maji ya kunywa ambayo yanauzwa Cedi Moja katika mikoa mingine lakini TAKORADI maji hayo yanauzwa kwa Cedi NNE, hali hii inawafanya wakazi wengi wa mji huu siku za mwisho wa wiki kwenda kununua bidhaa ACCRA “.( umbali wa saa 4 kwa gari ndogo kutoka ACCRA  mpaka TAKORADI)

Akizungumzia hali hiyo naibu waziri wa MKOA WA MAGHARIBI, ALFRED EKOW GYON amesema serikali inaendelea kuanzisha miradi mbalimbali na kushirikisha wananchi ili kuweza kuwainua kiuchumi pamoja na kutoa elimu ya wao kujiendeleza wenyewe kwenye miradi yao.

GYON pia ameeleza kuwa nivigumu kuwahudumia wananchi wote mkoani humo kutokana na watu wengi kutoka mikoa ya KASKAZINI kuhamia mkoani wakiamini watapata maisha bora zaidi.

Tayari taasisi mbalimbali zimeanzishwa ikiwemo WESTERN REGION COASTAL FOUNDATION ili kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujihusisha na masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo KILIMO na pia taasisi hiyo inachukua jukumu la kuwa mtu wa kati katika kuwasilisha malalamiko ya wananchi na majibu ya serikali kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment